18 Mei 2020 - 13:51
Ayatullah Raisi: Kukombolewa Quds ni moja ya mambo yanayopewa kipaumbele na Umma wa Kiislamu

Mkuu wa Vyombo vya Mahakama vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria hatua haribifu za Marekani na utawala haramu wa Israel katika eneo hili la Asia Magharibi na kusisitiza kuwa, kukombolewa Beitul-Muqaddas ni katika mambo yanayopewa kipaumbele na Umma wa Kiislamu.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Ayatullah Sayyid Ebrahim Raisi amesema hayo leo katika kikao cha Baraza Kuu la Vyombo vya Mahakama vya Iran ambapo ameeleza kuwa, baada ya kuangamizwa kundi la kigaidi la Daesh ambalo lilizaliwa na Uzayuni, utawala huo ghasibu unahaha ukitafuta njia ya kujiondoa katika hali ya kutengwa unayokabiliwa nayo.

Mkuu wa Vyombo vya Mahakama vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, njama za Marekani na utawala ghasibu wa Israel za kufanikisha mpango mchafu wa Muamala wa Karne na kupora ardhi zaidi za Wapalestina za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuziunganisha na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni maghasibu katu hazitafanikiwa.

Ebrahim Raisi amesema pia kuwa, Intidaha ya Palestina itazidi kuupata nguvu na kuwa kubwa kuliko Intifadha zilizotangulia.

Mkuu wa Vyombo vya Mahakama vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria baadhi ya jinai za utawala bandia wa Israel katika eneo hili la Asia Magharibi na kueleza kwamba, baada ya kupita miaka 72, hii leo faili la utawala huo limejaa jinai nyingi dhidi ya binadamu, ukiukaji wa mikataba yote na kupuuza haki za wananchi wa mataifa mbalimbali wakiwemo wa Palestina, Lebanon na mataifa yote yya eneo hili.